Feb 28, 2011

VITA WAISLAM NA WAKRISTO VYANUKIA.

Tabia ya kutoa kashfa kwa dini zingine huenda ikaangamiza umoja wa kitaifa.Wakristo Mjini Magharibi Zanzibar wameendeleza chokochoko dhidi ya wenyeji wao ambao ni waislam. Wakristo hao wanatoa kashfa kwa Waislam na Uislam kwa kumtukana Mungu na mtume Muhammad. Mbaya zaidi kama hawajaridhika waliamaua kukidhalilisha kitabu kitakatitifu cha Qur'an kwa kukichoma moto.Waislam walivumilia na kuamua kuzijulisha mamlaka husika pia na kuamua kumwandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.Lakini pamoja na juhudi hizo hakuna hatua madhubuti zozo zilizochukuliwa hadi sasa.Kutokana na hilo la wakristo kuachwa wakiudhalilisha Uislam,Waislam kwa kauli moja wameamua kutokulalamika tena bali nikuchukua hatua ya kuwaadabisha wafanyaji wa vitendo hivyo.Endapo wakristo wataendele basi vita kali huenda ikaripotiwa na hasara kubwa kutokea.Chokochoko hizi za kidini huenda zikaumong'onyoa kabisa muungano wa Tanzania,na tabia hii isipozuiliwa huenda ikaumong'onyoa umoja miongoni mwa raia na kusababisha maafa na kutoweka kwa amani nchini,kwani bado tuna kumbukumbu ya yale yaliyokea Mto wa Mbu kule Monduli mkoani Arusha. Serikali inatakiwa kuyafanyia kazi malalamiko ya kidini yote yanayo wasilishwa kwao kwani inaonekana kuna uzembe ama kutokujali. Hatua zisipochukuliwa Taifa huenda likatumbukia kwenye vita ya kidini na kuliangamiza Taifa kwani dalili ndio hizi.

Feb 27, 2011

MABOMU YALIPUKA SHINYANGA

Mabomu yaliyolipuliwa na jeshi Mkoani Shinyanga yamezua hofu. Hofu hizo zimetokana na wananchi ama kwa kupuuza au kutokuwa na taarifa sahihi,kwani jeshi lilikuwa tayari limetoa tangazo.Tangazo hilo kwa wananchi liliwafahamisha raia kuwa kutakuwa na ulipuaji wa mabomu. Maeneo ya Kizumbi ndio hasa yaliyokuwa kwenye hofu kubwa baada ya milio mizito kusikika.Baadhi ya wananchi walianza kukimbia ili kujìhami. Wengi walidhani yale ya Mbagala na Gongo la Mboto yamehamia Shinyanga. Baada ya ulipuaji huo hakuna maafa yaliyoripotiwa,kwani katika hofu mengi hujitokeza.WITO, Jeshi lihakikishe linasambaza taarifa kwa watu kwa muda mrefu kabla ya shughuli nzito kama hizi ili kuondoa hofu au hata maafa yasiyotarajiwa,kwani inaonesha watu wa Shinyanga hawakuwa na taarifa. Hata kule Gongo la Mboto taarifa zilitolewa mapema kuwa kuna kila dalili ya kulipuka mabomu ila inaonesha wachache ndio waliopata taarifa hizo,hivyo basi maafisa habari wa jeshi wanatakiwa kuhakikisha kwa njia zote taarifa zinawafikia wananchi.

ZIJUE SABABU ZA WATU KUTOKUPIGA KURA 2010.

Uchaguzi mkuu wa Tanzania wa oktoba 2010 ulikumbwa na tatizo la uchache wa wapiga kura. Sababu zipo nyingi zilizo sababisha uchache huo. 1. Baadhi ya wananchi kutokuwa na imani na viongozi wanaowachagua kwa madai ya kujijali wao wenyewe na kuwasahau wapiga kura wao.Hivyo wananchi hawakuona haja ya kwenda kupiga kura kwa kuwa wanaamini wanasiasa huomba kura kwa hoja nzuri lakini baadae huangalia matumbo yao "siwezi kupoteza muda wangu kwenda kupiga kura ili kumpa mtu ulaji akashibishe tumbo lake na familia yake,sina haja! Yoyote atakayeshinda kwangu sawa tu" haya ni maneno ya mwananchi mmoja aliye kubali kuwa hakupiga kura. 2. Baadhi walijiandisha na kupata vitambulisho kwa nia ya kuwasaidia katika mambo yao binafsi,mfano,kusajili namba zao za simu na kubwa ni kwa ajili ya kuchukulia mikopo katika taasisi za fedha na sababu zingine kwa kuwa hadi sasa hakuna vitambulisho vya kitaifa. 3. Taarifa zingine zinasema kuna baadhi ya wagombea walinunua vitambulisho vya kupigia kura na hasa vitambulisho vya wanaoonekana huenda wakawapa kura zao wapinzani wa wagombea hao.Kiukweli hili lilikuwa likituhumiwa sana kuwa ndio chanzo cha kupunguza idadi ya wapiga kura. 4. Uzembe wa baadhi ya wapiga kura wa kutokwenda kutazama majina yao kabla ya siku ya kupiga kura na ambapo kuna majina hayakuonekana kwenye kituo cha kupigia kura.Ambapo walitakiwa kwenda kabla kutazama majina yao na kama hayaonekani au yamekosewa walitakiwa kutoa taarifa ili marekebisho yafanyike. 5. Tume ya uchaguzi kushindwa kuhakikisha hakuna mwananchi aliye rukwa kwa kutazama na kulinganisha orodha kabla ya kuchapa na kutuma vituoni, hapa inaonesha kuna uzembe na kutokujali ambako kumesababisha baadhi ya wananchi pamoja na kuwa na vitambulisho kukosa haki yao ya kupiga kura. 6. Wananchi baadhi walikuwa wagonjwa siku hiyo pamoja na kupewa kipaumbele wanapofika katika vituo lakini wengi wao hawakwenda.7.Hofu ya kutokea machafuko na uvunjifu wa amani katika vituo nayo pia ilikuwa sababu ya baadhi kutokwenda kupiga kura. 8. Kukosekana kwa elimu ya uraia kwa baadhi ya wananchi ambao waliona hakuna umuhimu wa kupiga kura na wengine hata kusema"kura yangu moja haipunguzi wala kuongeza chochote" ambapo walisahau ule usemi usemao " kidogokidogo hujaza kibaba". Hizi ndizo sababu mimi nilizoziona,kwa ushauri wangu katika uchaguzi mkuu wa 2015 mianya hii izibwe ili wananchi wengi waweze kujitokeza kwa wingi kupiga kura,mfano suala la elimu ya uraia litiliwe mkazo sana. Wagombea wanaotoa rushwa na hongo ili kushinda, wakidhibitika wachukuliwe hatua kali ikiwa ni pamoja na kufutiwa haki ya kuwa mgombea maisha.

Feb 26, 2011

UDINI WA KIKWETE NI UPI?

Siasa za Tanzania zimetumbukiwa na nyongo tena nyongo kali. Nyongo hii ni Udini uliotawala ndani ya nyoyo za Watanzania, maranyingi nimesikia kuwa Rais Kikwete mdini na anawapendelea Waislam.Basi na tutazame na mwisho tuangalie huo udini uko wapi.Katika matamko kadhaa ya Waislam inaonesha kweli kunatatizo kubwa nchini mwetu. 2005 Kikwete alikuwa chaguo la Mungu kwa makanisa na maaskofu,wakristo kweli walimkubali,waislam nao walikubali baada ya kuahidiwa mahakama ya kadhi,mahakama ambayo itahusu mambo ya kiislam kama ndoa na mirathi. Baada ya ushindi wa Kikwete ilifuatiwa na uteuzi wa baraza la mawaziri.Baada ya uteuzi huo wiki chache baadae likazuka jambo na magazeti yakaandika kwenye kurasa za mbele. Kikwete ajaza waislam,baraza latawaliwa na waislam-hivi ni baadhi tu ya vichwa vya habari kwenye kurasa za mbele. Ikagundulika kuwa tatizo ni vitu viwili tu,navyo ni kardinali kuondolewa kwenye baraza la mawaziri, swali la kujiuliza alikuwa anaingia kwenye baraza kama nani? Hili likawakera maaskofu. Pili,kuondolewa kwa ubalozi wa papa Ikulu,swali ubalozi wa papa unangoja nini Ikulu na una mwakilisha nani na kwasababu zipi? Baada ya Kikwete kuhoji uhalali na kuondoa vitu hivi akawa adui mkubwa na kuwa si chaguo la Mungu tena mwaka 2010 na hata baadhi ya waumini wa kanisa kule Rukwa kufukuzwa kanisani na kufutiwa ushirika kwasababu tu walimpigia kura Kikwete. Kuibuka kwa hoja ya waislam kuipeleka Tanzania OIC na kurejeshewa waislam mahakama ya kadhi,vikao vilikaliwa na hata baadhi ya wachungaji na maaskofu kufikia hatua ya kusema 'damu itamwagika,endapo waislam watapewa mahakama na OIC'. Hivyo mpaka hapo utajua mdini ni nani! Ikulu ni ya Watanzania wote,baraza la mawaziri ni kwa ajili ya mawaziri wateule tu. Hoja na chuki zikapandikizwa miongoni mwa wakristo ili Kikwete awe sio kiongozi anayefaa,kwani tayari mambo na misheni za kanisa zinaonekana kuingiliwa. Kikwete akaitwa na anaitwa mdini na hafai kuongoza Taifa hili.Labda nikumbushe tu kuwa wakati Rais yeyote Muislam anapoongoza nchii basi atakumbana na hali ngumu kisiasa hata afanye mazuri hayaonekani na yeye huitwa asiye na akili. Mpaka hapo mdini ni nani? Turejee kampeni za uchaguzi wa Oktoba mwaka jana,ambapo udini ulionekana wazi japo wengine waliukana japo nyuso zao zinasomeka. Nchi hii niyetu sote Waislam na Wakristo basi na tuheshimiane ili kudumisha amani yetu. Mmoja mwenye nguvu amehodhi vitu vingi na yule dhaifu ana kidogo,anapotokea wakutaka kuweka angalau kupunguza tatizo basi mwenyenguvu huona anataka kupokonywa vyote hivyo mapambano hapo huanza. Udini udini upo sana lakini kwanini? Kigezo elimu? Hapana kwa kuwa sasa jamii karibu yote sasa inasaka elimu kwa nguvu. Sina ugomvi na dini yoyote,lakini hili ni tatizo.Mfano tulikuwa na jamaa zangu nikawaambia kwa hali ya siasa za Tanzania sasa CCM inahali ngumu 2015 labda wampitishe mtu anayekubalika kama Dr.Salim,wakang'aka yaani Muislam tena? Tumechoka! Nikagundua kumbe ni kweli mambo haya! Mahala popote panapokuwa na kiongozi wa juu Muislam huonekana hana uwezo na nafasi hiyo amepewa kwa upendeleo.Tabia hii ni mbaya. Niwazi kuwa kwa hayo yote ccm haiwezi kua chaguo bora kwa baadhi ya ndugu zangu. Niwazi kuwa mgombea wa chadema aliungwa mkono na makanisa na hata uelekeo wa kampeni na hadi sasa dalili zipo wazi.Yote haya yapo kwa ajili ya maslahi ya ukristo na wala sio Uzalendo wa Utanzania kwanza.Tukumbuke mwakajana Mh.Slaa inaarifiwa alilala parokiani mjini Arusha pia matamshi ya chadema kua'tutahakikisha nchi haitawaliki' hii inamaana kuna mbinu zitatumika na nyingine zinatumika kuuchafua utawala.Hili inawezekana kwa kuwatumia watu waliomo serikalini ili kweli ionekane Kikwete hawezi na hataweza kutawala nchi hii. Matamshi ya Mwanza ya Slaa pia yalinifanya nijiulize maswali pasipo majibu 'tunataka tuikomboe nchi' sasa tunaikomboa nnchi kutoka kwa Mafisadi au kutoka utawala unaodaiwa wa Kiislam? Kweli nchi imemezwa na mdudu ufisadi na nihaki kwa kila mtu kuupiga vita kubwa,na tutambue fisadi hana dini. Kama kumpiga vita Kikwete kwa sababu ya ugumu wa maisha na ufisadi hapo sawa ila sio kwa dini yake. Udini wa Kikwete mimi siuoni na kama upo basi uleteni hapa na sote tuujue. Maandamano yanayoitishwa nchi nzima huenda yakatutumbukiza kwenye maafa ya kidini na sio kisiasa. Nasema hivi kutokana na harufua au uelekeo wa siasa za Tanzania. Tukija kwa upande wa chadema ambacho kinaungwa mkono na makanisa hili ni doa kwao chadema kwani ndani yake udini unaonekana wazi,wote tunakumbuka mwaka jana Zito Kabwe alitaka uenyekiti lakini akakataliwa mwisho wazee wakamsihi atulie naye akawasikia,nikakumbuka ile kauli ya rafiki zangu ya "muislam tena? Tumechokt",kwani ilikuwa wazi Zito angeomba urais na angepata urais misimamo ya upendeleo hakubaliani nayo hivyo angeenda haki tu! Lakini pia kumsimamisha mgombea mwenza katika nafasi ya urais mhitimu darasa la saba, haya yalikuwa matusi na dharau kwa Waislam Watanzania wote na kuwaonesha kuwa wao hawana elimu hivyo wanastahili kupewa tu nafasi za upendeleo tu.

Feb 24, 2011

MAMIA WAANDAMANA MWANZA

Kama unavyoona picha namba moja hadi namba tano hapo juu ni umati wa watu wakiwa wamehudhuria maandamano makubwa ya chadema jijini Mwanza.Picha zote zinaonesha umati ukiwa umetulia ukisikiliza kwa makini na wakati mwingine wakishangilia sana.Meya wa jiji alizomewa na mamia ya wahudhuriaji kwa madai ya kununuliwa na ccm na kuwasaliti wamachinga.Dr Slaa alipopanda jukwaani pia naye alionesha kuitikia linalosemwa na wapiga kura kua hawamtaki Mh.Josephat Manyerere ambaye ni meya wa jiji kwa kusema atamfuatilia kwa karibu zaidi kwani 'hatukukuita Dodoma na Dar es salaam bure' alisema Mh.Slaa. Naye mbunge wa Ilemela Mh.Highness Kiwia lisema ccm wamemuundia kesi kwa tuhuma za kutumia lugha za vitisho wakati wa kampeni na kununua kadi za kupigia kura. Pia Dr.Slaa amempa siku tisa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Jakaya M.Kikwete ili atoe tamko la serikali kuhusu Dowans,mfumuko wa bei na kulipuka kwa mabomu Mbagala na Gongo la Mboto la sivyo atatoa tamko. Vilevile amewataka Mawaziri wawili kujiuzuru kutokana na uzembe wao,mawaziri hao ni waziri Ngeleja na Hussein Mwinyi. Akihitimisha mkutano huo mkubwa Mh.Mbowe aliwauliza wahudhuriaji wanataka ya Misri na Tunisia? Wote wakakubali kwa sauti 'tunatakaaa'. Pia akaongeza kuwa maandamano hayo yataendelea katika mikoa yote ya kanda ya ziwa 'tunaenda kwenye wilaya zote,tukitoka hapa ni Ukerewe,tutagawana maeneo yote.Baada ya Mwanza ni Mkoa wa Mara na wilaya zake kisha Kagera,Shinyanga,Tanga,Dar es salaam,...'Mpaka kieleweke.Alisema Mh.Mbowe.Mwisho raia walitawanyika kwa amani na kurudi makwao.Baada ya kutawanyika baadhi ya wananchi walionesha hofu juu ya matamshi ya viongozi wa chadema kuwa yanahamasisha fujo. Wakitoa mfano wa kauli ni kama ile ya Dr.Slaa kuwa ni bora kuishi miaka mitano kuliko kuishi miaka mingi na ukafa kwa tiphord itakuwa aibu mbinguni. Wakati huohuo yamezuka mapigano makali kati ya Waislam na wakristo huko Mto wa Mbu mkoani Arusha.Hadi sasa ripoti zinasema makanisa kadhaa yameharibiwa.Chanzo cha vurugu inasemekana ni mkutano wa mhadhara wa wakristo uliokua unatumia Qur'an na Biblia ambapo Waislam waliona kuna kashfa,matusi na kejeli za wazi kwa Mwenyezi Mungu(ALLAH) na Mtume Muhammad(s.a.w) ndipo walijiunga na kuwavamia wakristo,hadi tunaingia mitamboni wachungaji wawili wamedhibitika kujeruhiwa na askari wakijitahidi kurudisha amani.

Feb 23, 2011

CHADEMA WAVAA MAGWANDA DARASANI.

Wanachama sugu na viongozi wa chadema tawi la Chuo kikuu cha Mt.Augustine(SAUT) Mwanza leo wametinga madarasani kuhudhuria mihadhara(lectures) wakiwa ndani ya sare(uniform) za chama chao. Wanachama hao na wapenzi wafuasi wa chadema wameonekana chuoni hapo na mavazi yao huku wanachuo wengine wakibakia kushangaa. Baada ya kufuatiliwa nyendo zao na kuhojiwa walisema hiyo ni njia moja wapo ya kuhamasisha watu kuwaunga mkono katika maandamano yatakayofanyika kesho jijini hapa.Maandamano hayo imefahamika rasmi kuwa yataanza saa saba mchana,na yakianzia Standi ya mabasi ya Buzuruga hadi viwanja vya wazi vya Furahisha maeneo ya Kiruba jijini Mwanza.Lakini baadhi ya watu wameonesha kuwa na wasiwasi wa kushiriki maandamano hayo kwa kuhofia kupigwa mabomu na risasi za moto. Pia wengine wamedai kua kesho ni siku ya kazi hivyo muda huo watakuwa wako kazini hivyo wao walipendelea ingekuwa Jumamosi au Jumapili.Mmoja wa viongozi wa tawi la chuo cha SAUT aliulizwa juu ya hofu ya mabomu alisema"tunajua wazi kuwa mabomu yatakuwepo ila sio yale ya Mbagala na Gongo la Mboto hivyo tutaandamana,lakini kwa amani".

Feb 22, 2011

GADDAFI SASA MBIONI KUNG'OKA

Rais wa muda mrefu nchini Libya Kanali Moammar Gaddafi muda si mrefu atang'oka madarakani.Hii imetokana na dunia kumshangaa kiongozi huyu kuamrisha wanajeshi kuruka na ndege za kivita dhidi ya waandamanaji na kuwarushia mabomu. Kutokana na mabomu hayo ambayo yameua watu wengi hadi sasa duru za kimataifa zimeanza kufananisha na mauaji ya kimbali.Hadi sasa watu wapatao 400 wameripotiwa kupoteza uhai,japo idadi kamili bado haijajulikana kwani pia risasi za moto zinapigwa kwa raia hao wanaoandamana kwa amani kumtaka Gaddafi kuondoka madarakani kama Mubarak na Ben Ally.Vuguvugu la maandamano kuwang'oa watawala katika nchi za kiarabu limeshika hatamu ambapo imebidi umoja wa nchi za kiarabu kuitisha kikao cha dharura ili kujaribu kuweka mambo sawa. Kutokana na hali kuwa mbaya sana nalo baraza la usalama la umoja wa mataifa limeitisha kikao ili kudhibiti mauaji yanayoendelea. Wakati huohuo mabalozi wa Libya walioko barani Asia wamejiuzulu kupinga mauaji yanayoendelea nchini Libya, na hapa sasa inaonesha mwisho wa Gaddafi umefika. Kutokana na mauajia haya ya raia wasio na hatia Gaddafi baada ya kung'olewa huenda akashtakiwa katika mahakama ya kimataifa huko nchini Uholanzi katika mahakama ya The Hague.Mwisho,tuwaombee kila dua njema ndugu zetu wa Libya waweze kufanikiwa katika lile wanalopigania na pia kuwaombea kwa Mungu wale waliouawa pia na majeruhi ili wapone haraka."MUNGU wape faraja na Amani watu wa Libya"AMIIN.

Feb 21, 2011

CHADEMA KUANDAMANA MWANZA

Chama cha demokrasia na maendeleo(chadema) wamepanga kuandamana tarehe 24Februari,2011.Maandamano hayo yanayotarajiwa kua ufuasi mkubwa sikuhiyo kutokana na chama hicho kuwa na wafuasi na wapenzi wengi jijini hapa.Viongozi wa juu wa chadema wanatarajiwa kuongoza maandamano hayo yaliyopangwa kuanzia stendi ya Buzuruga na kuishia kwenye uwanja wa wazi wa Furahisha uliopo Kirumba jijini hapa.Lengo kuu la maandamano hayo ni pamoja na kushinikiza Rais Kikwete ajiuzulu,kupinga mambo mbalimbali kama kupanda kwa gharama za umeme,kupinga ufisadi,kupinga Dowans kulipwa na kuongezeka kwa gharama za maisha.Kutokana na ughali wa maisha nchini maandamano hayo huenda yakasimamisha shughuli nyingi mjini na watu kwenda kuunga mkono maandamano hayo yanayotarajiwa kuanza mishale ya saa nne asubuhi.Wimbi hili la maandamano huenda likaenea mikoa yote ambayo inawafuasi wengi hasa wa upinzani.

Feb 19, 2011

MAJONZI KWA WATANZANIA.

Majonzi makubwa yametukumba tena watanzania.Mabomu yaliyolipuka Gongo la Mboto jijini Dar es salaam kwenye ghala la JWTZ la silaha limesababisha vifo na majeruhi mengi,kwani hii imetutonesha vidonda vya mabomu ya Mbagala ambayo yalisababisha maafa makubwa pia. Kidau inawafariji wahanga wote wa kadhia hiyo na kuwapa pole pamoja na dua kwa Mungu.Mungu atufanyie wepesi katika haya mazito na kutufuta machozi kutokana na majonzi haya."Eee Mungu wenye majeraha uwaponye kwa nguvu zako na waliopoteza ndugu basi wajaalie waonekane ili nyoyo zetu zifarijike".Ee Mungu tupe faraja nyoyoni mwetu na utujaalie Amani katika miji yetu, utubariki kwa mvua na mazao.Aaaamin.

Feb 16, 2011

RAIS WA CHUO CHA SAUT ANG'OLEWA.

Ndugu Patrice Jisebo Rais wa chuo cha Mt.Augustine cha jijini Mwanza ameng'olewa madarakani akiwa mwishoni mwautawala wake imefahamika.Kung'olewa kwa Rais huyo kumetokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo ya kupokea na kuomba rushwa ili atoe huduma,pia alituhumiwa kwa ukabila katika serikali yake pamoja na utendaji usioridhisha.Tuhuma nyingine ni kuwa inasemekana alikula fedha ya ada ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na kusababisha ashindwe kufanya mitihani yake ya semester ya kwanza.Mengine ni kushindwa kusimamia masuala ya mikopo ya wanafunzi hivyo kusababisha wanafunzi wengine kuteseka kwa ukosefu wa fedha baada ya taarifa zao kucheleweshwa kwenda Bodi ya mikopo ya elimu ya juu.Pia imefahamika kua ameshindwa kusimamia ratiba ya chuo kwani mfano mitihani ya semester ya kwanza ilipaswa kuisha tarehe 30 January 2011 na masomo ya semester kuanza tarehe 1February lakini ghafla ratiba ilibadilishwa kwa baadhi ya masomo kuendelea hadi tarehe 5February ,hivyo kusababisha wengine kukosa vipindi wakati wengine wakiendelea na masomo.Aidha chanzo chetu cha kuaminika toka chuoni hapo kwa wasomi wanaotegemewa na taifa zinaendelea kubainisha kuwa ofisi ya rais huyo imekua ikivamiwa na wanafunzi kana kwamba hakuna mawaziri ili kupata ufafanuzi wa mambo mbalimbali hasa yale yanayohusiana na mikopo pia yeye mwenyewe rais imemlazimu kuwaondoa mawaziri katika nyadhifa zao hususan wale wa mikopo ambapo wakwanza na wapili wote waliondolewa kwa nyakati tofauti kutokana na utendaji duni.Viongozi hao walioondolewa na rais ni pamoja na Marwa aliyekua waziri wa kwanza wa mikopo akifuatiwa na Buchwa ambaye pia alisimamishwa kwa utendaji mbovu na wote wakihusishwa hasa na rushwa pamoja na majibu mabaya kwa wanachuo.Kikao cha Bunge la wanafunzi ambao walipiga kura ya kutokua na imani na rais ambapo asilimia 78 wote hawakua na imani naye kutokana na hilo madaraka ya urais alipatiwa aliyekuwa makamu wake,ambaye atakua rais hadi uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwezi Machi hatahivyo imefahamika kuwa aliyekua rais ndugu Jisebo ambaye yuko Elimu mwaka watatu amepoteza sifa ya kutunukiwa cheti cha sifa ya urais wa SAUTSO akiwa chuoni hapo.SAUTSO ni serikali ya jumuiya ya wanachuo wa St.Augustine University.Baada ya taarifa za kung'olewa kwa rais huyo wanachuo wengi walifurahi na wachache baadhi walihuzunika kwa sababu mbalimbali.Baadhi ya wanachuo walipongeza uamuzi huo wa wabunge wao wa kikao cha tarehe 13 February ila wakasema kua kama hawakuwa na imani na rais basi serikali yote ingeng'olewa na kuwekwa ya mpito hadi uchaguzi wa mwezi machi.

Feb 15, 2011

MGOMO WA DALADALA MWANZA

Siku ya leo imekuwa ngumu kwa wakazi wa Mwanza baada ya magari ya abiria aina ya daladala kugoma kutoa huduma.Watu wenye shughuli zao katikati ya jiji wanaotoka maeneo mbalimbali walikuwa na wakati mgumu baada ya kukusa huduma hii muhimu ya usafiri.Wanafunzi ndio walikuwa na hali mbaya zaidi kwani baada ya masomo walilazimika kutembea kwa miguu,huku wengine wakiwa na njaa kali kutokana na hali ya maisha kua ngumu. Wamiliki wa magari ya daladala wamegoma ili kuishinikiza sumatra iwakubalie kupandisha nauli kutokana na bei ya mafuta kupanda. Leo magari ya watu binafsi yasiyo kwaajili ya kusafirisha abiria yalitumika kusaidia kuwapeleka na kuwarudisha abiria ndani na nje ya jiji la Mwanza kwa bei ya Tsh500 hadi 1000. Mgomo huu umeleta adha kubwa kwa watu wa kipato cha chini waishio nje kidogo ya jiji la Mwanza na vitongoji vyake, kwani iliwalazimu wengine kutembea kwa umbali mrefu ili kwenda kuusaka mkate wao wa kilasiku.Tunaiomba sumatra walitazame hili haraka ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Feb 13, 2011

YA MISRI TANZANIA HAYAWEZEKANI.

Wote tumekuwa mashahidi kwa kile kilichojitokeza nchini Misri na Tunisia kuwa wananchi wa nchi hizo wakiwa na nguvu moja na sauti moja wakiwafurusha madarakani madikteta walio kaa madarakani takribani miaka 30. Haya ni mapinduzi makubwa ya kidemokrasia kwa nchi hizo,lakini wimbi hili halitaishia Misri na Tunisia bali wimbi hili huenda likazikumba baadhi ya nchi za Kiafrika na za Kiarabu pia.Nchi kama Libya,Sudan,Zimbabwe na Uganda huenda zikaishia kwenye nguvu ya umma pia ili kuwang'oa ving'ang'anizi wa madaraka.Rais Hosni Mubarak wa Misri na Ben Ally wa Tunisia wote wameng'atuliwa na nguvu ya sauti moja ya raia wa nchi hizo.Je,hii pia inaweza kuipata Tanzania? Swali hili linahitaji kujadiliwa kwa kina,huu ndio mtazamo wangu kua haiwezekani kutokana na sababu zifuatazo; 1. Tanzania nia yetu haiko wazi kwani watu wana malengo yao na agenda zao tofauti.Hapa tofauti na agenda za udini zimejionesha wazi hivyo kuwagawa wananchi kwa misingi hiyo.Hivyo wananchi kuvunjiwa umoja wao.Wanasiasa kukana kua hakuna udini Tanzania ni sawa na kuuficha moto kwa viganja ilihali moshi unaonekana"ukificha moto moshi utakuumbua" usemi huu umedhibitika juzi baada ya viongozi wa dini kukutana pale Mövenpick na kujadili mustakbali wa amani Tanzania.Kwani wao waligundua kua udini huu utaliangamiza Taifa letu na kua kisiwa cha vurugu badala ya Amani tuliyoizoea.Kwa agenda hii kua kama Misri na Tunisia ni ngumu,kwani huenda tukaishia kuuana wenyewe kwa wenyewe. 2. Agenda ni kumng'oa Kikwete au kuing'oa CCM? Hapa mimi sielewi vema.Kama sababu ya kuhamasishana kuandamana na kugoma ni Kikwete atoke madarakani hapo pia tumeshashindwa kabla ya kuanza au kuendelea kwa nguvu,sababu ya msingi ya kumng'oa ni Uislam wake au ufisadi uliopo tangu enzi? Sote hatupendi ufisadi basi sote tusimame pamoja kuupiga vita,lakini mbona pia hapa kuna udini pia? Binafsi nimezungumza na wengi na kuhojiana nao wakidai "hatumtaki Rais muislam" ha! hili limetoka wapi?Nilishangaa na mwisho nikagundua kua kumbe tatizo sio CCM bali ni uislam wa rais. 3.Kama nia ni kuing'oa CCM na mfumo wa utawala hapo sawa! Lakini nia ya dhati ipo?mbona wapinzani hampatani? Wafuasi tumsikilize nani? Tayari huu ni mgawanyiko mwingine unao watenga raia,hivyo kuifanya dhana ya kuing'oa serikali kua ngumu. 4. Kama suala la udini litaendelea na kubezana kidini basi tumepoteza welekeo na lengo la maendeleo itakua ndozo za alinacha.Mgawanyiko huu mkubwa hauna uwezo au nguvu ya kuleta mabadiliko kwani siasa zetu sasa zimeelemewa na hisia kali na ushabiki wa hali ya juu,na bila shaka palipo na ushabiki kuna pande mbili pinzani na mwisho wa ushabiki mkali ni kuumizana. 5. Kuwepo kwa viongozi wa CCCM wanaoungwa mkono na wapinzani pia hili ni tatizo! na hii ndio inadhibitisha kua kuna agenda ya nyuma yake.Hivyo aking'oka Kikwete na wakashika madaraka wale tunao wakubali basi naona kwa agenda hii maandamano wala mapinduzi hakuna.Kwa wale wenye subira ngoja tuone 2015 kitakachotokea. Lakini kwa ubinafsi na udini hatutaweza hadi tuwe na nia na lengo moja watanzania wote. Kwa sababu hizi basi yaliyojitokeza Misri kwa Tanzania haiwezekani.Kama nia ni kuiondoa ccm nilazima wapinzani wawe wamoja na wawe na lengo moja tu. Maisha magumu sote tunaugulia, hasa sisi tulio chini mfano wamachinga,wakulima na hata wafanyakazi waaminifu na mwisho ni wale wasio na hata vimitaji pia na elimu. Kama tatizo ni UFISADI na UMASIKINI hapa Watanzania wote tutakua pamoja hadi ushindi upatikane na nafuu tuipate ila sio agenda za udini na uchama.

Feb 10, 2011

UTAJUA UMUHIMU WA KITU BAADA YA KUKIPOTEZA.

Hakika mimi nasema "huwezi kujua umuhimu na thamani ya kitu hadi kipotee".Je,tiba ni bora kuliko kinga? Ukitunza sindano mahala kisha bila kuithamini ukaweka bila kutazama ulipotunza eti kwa sababu nguo zako zote ni mpya,huna sababu ya kuitunza vema kwavile hutarajii kuitumia hiyo sindano.Nguo mpya lakini leo imetatuka na sindano hujui wapi ulipoiweka kwakuwa mwanzo haikua na thamani wala umuhimu sasa una anza kuisaka kwa kung'uta maguo na kufagia ili uipate kutokana na umuhimu wake.Baada ya kutatukiwa ndio unaona umuhimu wa sindano? Kweli umuhimu wa kitu ni hadi kipotee.Wanafunzi shuleni kila waaswalo wao hawafikiri mwisho huishia na kupata sifuri,hii ni kwa vile hawakujua thamani ya muda.Kurudia mitihani hii inaonesha mwanafunzi anatafuta alichopoteza wakati uliopita kwani wakati huo hakujua thamani na umuhimu wa masomo.Kweli thamani ya kitu huwezi kuijua mpaka kipotee.Kupotea kwa amani kunakoonekana sasa nchini tukuja kujuta na kuuguza vidonda kwani hii inaoneshwa na chokochoko zinazoendelea.Amani thamani yake kubwa,tusingoje kwenda kuitafuta mezani na p.o.p na bandeji na chongo na vilema, basi na tuone thamani yake na tuitunze. Kweli thamani ya kitu huwezi kuijua mpaka kwanza kipotee! Mfano unapesa nyingi kisha ukazifuja,vipi siku zimeisha na huna hata senti mfukoni? Thamani ya kitu huwezi kuijua mpaka kwanza kipotee. Amani kwa Watanzania ni jadi vipi leo?

Feb 8, 2011

HII NI AIBU KWA CHADEMA NA UPINZANI

Kitendo kilichofanywa na CHADEMA Bungeni mjini Dodoma ni aibu kwa chama chenyewe na upinzani kwa ujumla.Kitendo cha kukataa kanuni za bunge zisibadilishwe ili wapinzani waungane ni cha aibu na hii inaonesha CHADEMA wana agenda ya siri.Binafsi sileti ushabiki wa vyama ispokua nataka Watanzania watambue kua ubinafsi unatumaliza.Kama si ubinafsi leo tusingekua na ufisadi,nia na madhumuni kua na upinzani ni kuleta changamoto kwa serikali inayokuwa madarakani.Kugawanyika kwa wapinzani ni aibu kubwa sana ambayo haitafutika katika historia ya nchi yetu.Kukataa kwa chadema wenzao wa cuf,nccr,tlp na udp kujiunga nao katika kambi rasmi ya upinzani bungeni inaonesha chadema ni wabinafsi na hawapendi wapinzani kua na sauti moja.Je,hawa wapinzani walio nje ya kambi watakua upande gani katika suala la upinzani bungeni? Iko wazi wao wako radhi kuungana na chadema ili lao liwe moja nalo ni kua na msimamo mkali wa pamoja juu ya serikali.Kwa hoja ya cuf kuungana na ccm Zanzibar ambayo chadema kwao ndio hoja kuu, kwangu mimi hii haina mashiko.MOJA-Inaonekana kua machafuko ya Zanzibar chadema wanayapenda na amani ya Zanzibar wanaichukia,kwani lengo la cuf Zanzibar kukubali umoja nikutokana na wingi wa wafuasi wa ccm na cuf ambako imeleta mgawanyiko mkubwa na maafa hivyo ili kuwanusuru raia na roho zao ilibidi cuf kukubali kugawana madaraka.CUF Tanzania bara inajitegemea na ndio maana ina mgombea urais wake na Zanzibar mgombea wake.Hali ilivyokua Zanzibar ni hali ambayo Watanzania wote wapenda amani tuliichukia na kuombea siku moja amani ya kudumu inapatikani.Swali ni je,kwanini chadema wanakataa kuungana au kuna agenda iliyojificha.Haya tunasema hatutaki muungano na cuf kwa kuwa wao na ccm lao moja je,hawa waliobakia nao wako kwenye maridhiano na ccm? Kuna agenda gani ya siri inayowafanya kukataa kukubali madiliko ya sheria za bunge? PILI-Kauli ya Mh.Lissu haikua ya kiungwana kwani matamshi juu ya ndoa ya wake wengi na ile ya wanaume wengi ni dharau kwa watu wa Zanzibar hivyo mi naona ni vyema akaomba radhi kwa kauli hiyo.TATU-Kwa maana hii ile ndoto ya wapinzani kua na muungano wenyenguvu ili kuing'oa ccm inatoweka taratibu kwa kua na mgawanyiko mkubwa kama huu unaoonekana.NNE- Kama kanuni za bunge zilikua hazitafsiri vizuri kambi ya upinzani iweje,sasa ni wakati wa chadema kukubali ili wapinzani wawe wamoja.MWISHO-Kutoka bungeni kwenye bunge la kumi kwa chadema ni aibu.Mara ya kwanza tuliona labda ni sawa lakini kwa hili la leo la kutoka tena ili kukataa kanuni ya kuwaunga ni AIBU KUBWA.

Feb 7, 2011

VIONGOZI WA DINI KUKUTANA.

Viongozi wa dini Tanzania kukutana katika hotel ya Movenpick siku ya tarehe 9 mwezi february.Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa maandalizi Alhaji Alhad Mussa Salum ambaye ni Sheikh wa mkoa wa Dar es salaam BAKWATA.Mada kuu itakua ni mustakbari wa amani Tanzania,mkutano huo utawakutanisha Masheikh,Maustadh,Maaskofu na wachungaji.Hata hivyo hakuta kuweko na waalikwa au wataalam kutoka nje ya nchi.Mada hiyo kuu ambayo ni mustakbari wa amani Tanzania na nafasi ya viongozi wa dini inatarajiwa kuleta usawa na kuridhiana baina ya wanadini baada ya kuonekana mgawanyiko wakati wa uchaguzi mkuu wa oktoba mwaka jana.Mwenyekiti wa maandalizi pia aliwaomba waalikwa wote kufika ili kufanikisha mkutano huo.

Feb 6, 2011

AJALI YA MOTO

Kama unavyoona picha no.1 na no.2 hapojuu.Picha no.1 watu wakishangaa nyumba inayozimwa moto na no.2 ni gari la zimamoto maarufu kama fire.Ajali hiyo imetokea leo saa9 alasiri ambapo chanzo ilikua matairi na uchafu uliokua unachomwa kiambazani ambapo kulikua na shimo la taka.Nyumba hiyo ambayo ni Guesthouse na bar maarufu kama Kashonge iliyopo mitaa ya Nyakabungo(maarufu Genge la Mbuzi) wilani Nyamagana jijini Mwanza.Kutokana na msongamano uliopo kama moto huo ungesambaa ungesababisha hasara kubwa,hata hivyo gari la zimamoto liliwahi kufika mapema na kuonesha ni jinsi gani wanapenda na kujali kazi yao kwani leo ni jumapili.Mpaka tunaingia mitamboni ilikua bado haijajulikana hasara hasa iliyosababishwa na moto huo.

Feb 5, 2011

MH.KIKWETE HAPO UMENENA

Wakati Rais wa jamhuri ya muungano ya Tanzania Mh.Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa CCM nilifurahishwa na kauli yake ya kutaka Watanzania kuheshimiana katika maoni.'Msiwazomee wenye mawazo tofauti na ninyi' alisema Rais,kwani kiukweli ni kuwa hakuna kuvumiliana wakati wa kutoa maoni hususan katika mijadala ya kitaifa Rais alisema 'kutofautiana katika mawazo ni kawaida'.Tukirejea mjadala wa katiba uliofanyika katika ukumbi wa Nkurumah katika chuo kikuu cha Dar es salaa ambapo mtu aliyetoa maoni tofauti na mapenzi ya wengi alizomewa. Kwa wasomi kutofautiana kimawazo ni kawaida si kila hoja ya mwenzako ni sahihi au haiko sawa.Wasomi tunapojadili mambo ni sawa kutokukubaliana kutokana na vigezo vinavyokubalika na akili(logical) na pia hata sheria,hivyo kwa wasomi ukweli na halihalisi ndio hutawala nasio ushabiki na kujiwekea misimamo isiyobadilika(conservativism).Wasomi si (conservative) bali hukubaliana na hoja za kiakili (logical reasoning).Basi kwa msomi ambae hachambui vema na kuchukulia ushabiki kilajambo huyo hajaelimika na naweza kusema uwezo wake wa kuchanganua mambo ni mdogo.Mi namuunga Mkono Rais kwa kauli zake alizozitoa kwenye maadhimisho hayo ya kua 'tuvumiliane'.Basi na mimi nitumie nafasi hii kuwaomba watanzania kua kama hukubaliani na mawazo au mtazamo wa mwenzako,basi yaheshimu yale aliyoyasema na si kwa vile yuko tofauti na wewe basi azungumzalo kwako ni pumba.Msomi akizungumza pumba(pointless) lazima tumshangae basi tumpinge kwa hoja za kiakili(logica reasoning) na huo ndio usomi na kuelimika.

Feb 2, 2011

MBOWE NA CHADEMA MNATUCHANGANYA.

Mwenyekiti wa chadema taifa Mh.Freeman Mbowe jana tarehe 1/2/2011 alitoa kauli inayowachanganya wafuasi wake.Mwenyekiti huyo alitoa kauli ya kumtambua Rais ambaye mwanzo walisimama na kutangaza kutomtambua Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na hata kuungwa mkono na wapenzi na wanachama.Mh.Mbowe aliyasema hayo wakati wa kuadhimisha siku ya mahakama,ambapo Rais naye alihudhuria maazimisho hayo.Ikumbukwe kua msimamo wa kutomtambua Rais ulionekana dhahiri pale wabunge wa CHADEMA walipotoka nje wakati wa hotuba ya Rais kwa bunge."kisheria tunamtambua Rais".Swali langu ni kuwa ,pale mliposema hamumtambui rais sheria haikuwepo? Wakati wa mjadala wa bunge juu ya hotuba ya Rais,wabunge wa CHADEMA wangechangia? Sasa CHADEMA wanatuchanganya kutokana na sitaki na taka yao.Katika hotuba ya rais kuna vitu vya muhimu wabunge kujadili ambayo ni kwa maslahi ya Taifa!CHADEMA nadhani hili walilitambua na ndio maana wakaona kua wapole, je mwanzo hawakufikiri? Sasa hii inaonesha wazi kua Mh.Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma kaskazini pamoja na wabunge wengine wachache wa CHADEMA walikua sawa kukataa kutomtambua Rais na kutotoka bungeni(hawakuingia kabisa bungeni) pia inaonesha kua chama kinaongozwa na jazba na kamasivyo mbona kauli zinatoka za kujichanganya? Kwa maana hiyo CHADEMA wamelamba matapishi yao kwa kumtambua Rais ambaye mwanzo hawakumtambua.CHADEMA kueni na kauli thabiti ili kuepuka kuwaweka njiapanda wanachama na wapenzi wa chama.